KILIMANJARO serikali mkoani
Kilimanjaro imeombwa kutoa ushirikiano kwa wasanii waliopo mkoani Kilimanjaro
ili kuinua tasnia ya filamu mkoani Kilimanajro sanjari na kusaidia kukuza vipaji
vya waigizaji na kushirikisha sanaa hiyo ambayo imeonekana ikipuuzwa mkoani
Kilimanjaro.
Ombi hilo limetolewa na katibu wa
chama cha waigizaji na wacheza picha jongefu mkoani Kilimanjaro, Ditram
Ngonyani wakati wa mkutano mkuu wa kupitisha katiba ya chama hicho ambayo
iliwashirikisha viongozi wa chama hicho kutoka katika wilaya zote za mkoani
Kilimanjaro.
Ngonyani alisema mara nyingi
wasanii wamekuwa wakikosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa serikali waliopo
kwenye wilaya hususani maofisa utamaduni, jambo ambalo linazorotesha tasnia
hiyo na kuiomba serikali kutoa ushirikiano ili kukuza utamaduni katika wilaya
husika.
Amesema wakati mwingine maofisa
utamaduni wamekuwa wakitoa kauli chafu kwa viongozi wa chama hicho kauli ambazo
zimekuwa zikiwafanya kuonekana kutothaminiwa na serikali huku wengine
wakipuuzwa pindi wanapoomba kukutana nao.
Katika hatua nyingine katibu huyo
amewataka wasanii wanaoigiza kuvaa mavazi yenye heshima ili kuitangaza tasnia
hiyo na kuacha kuvaa nusu uchi kutokana na hatua hiyo kuwa ni ya
kidhalilishaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama
hicho, Ramadhani Msasu, ameiomba serikali kupitia wizara ya habari, tamaduni na
michezo kuacha kuwathamini wanamichezo wa mpira wa miguu zaidi na badala yake
kutoa agizo kwa maofisa utamaduni wote kutoa ushirikiano kwa vyama vya sanaa
kwani wao ndiyo wanaotangaza utamaduni wa mtanzania.
No comments:
Post a Comment