Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, July 9, 2014

VIONGOZI WA DINI MSICHOKE KUHUBIRI AMANI - SITTA


VIONGOZI wa dini nchini wametakiwa kutochoka kuwaasa waumini wao kufuata misingi na taratibu zao za kiimani ili kuepusha vurugu, machafuko na matendo mengine maovu na hatimaye kuifanya serikali kuwa na nafasi nzuri ya kufanya shughuli za kimaendeleo kwa faida ya wananchi.

Waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki Na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, alisema hayo wakati akizungumza na waumini wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) , usharika wa Ifakara wilayani Kilombero, alipohudhuria ibada kanisani hapo, iliyokwenda sambamba na tukio la uzinduzi wa albamu ya video ya nyimbo za injili ya Wakati wa Bwana ya msharika wa kanisa hilo Eva Mlwati katika uwanja wa Taifa uliopo wilayani humo.

Sitta mbali na kueleza kuwathamini viongozi wa dini na waimbaji wa nyimbo za injili wa Tanzania na Afrika Mashariki wanaoeneza amani kwa njia ya uimbaji, alisema Serikali inategemea zaidi mchango wa viongozi wa dini kuliweka taifa kwenye hali ya amani na utulivu na kwamba kiongozi yeyote wa kisiasa asiyeamini katika dini, hawezi kuwa kiongozi mzuri.

Katika mahubiri yake kanisani hapo, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Ulanga-Kilombero, Rainard Mtenji, pamoja na kuwataka wakristo kuiga mfano wa mtume Petro, kwa kutumia nafasi yao kiimani kusali na hata kuliombea taifa kupata katiba bora bila kusababisha uvunjifu wa amani au mgawanyiko wa watanzania, aliwataka kutenda mema na kuacha kuwatendea wengine yale ambayo hawapendi kutendewa.

Askofu Mtenji alisema inasikitisha kuona mwanamke alitegemewa kama mlezi wa familia kwa sasa amegeuka na kuwa katili kwa matendo yake, ikiwemo kuwafanyia ukatili watoto waliowazaa ama kupewa jukumu la kuwalea, kama kuwachoma moto, kuwanyima chakula na malezi bora, jambo ambalo linaipeleka dunia katika hali mbaya inayohitaji zaidi maombezi,na kwamba hali ya ukatili ilionekana zamani kufanywa na wanaume kwa kiasi kidogo na sio wanawake.

Alisema bado viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuendelea kuwavua watu kwa kutumia neno la mungu,kazi ambayo kanisa limekabidhiwa kuifanya, sambamba na jambo jingine muhimu sana la utunzaji wa wale wanaowavua, ili waweze kuishi maisha mema .

“Na hii sasa ni changamoto sio tu kwa kanisa, bali na taasisi nyingine, sio kama tunahitaji kuwa na watu wengi sana tuliowavua, bali inafika wakati unapaswa pia kuangalia ubora wa kile unachokivua,kwa sababu mwisho wa safar wa hao waumini, ni uzima wa milele, kwa hiyo pamoja na kujali wingi wetu, lakini pia tunapaswa kujali ubora wa hao waumini,kwahiyo katika kuwapima kiimani, tunapima pia matendo wanayotenda”Alisisitiza Askofu Mtenji.

Alisema mkristo hawezi kuwa mkristo kama hataongozwa katika vielelezo vya kutenda mema, na kuwaasa kujijenga katika maarifa ikiwemo ya kumjua Mungu na kuacha dhambi, alionya ni vyema kutowatendea wengine yale yote ambayo hata wao hawapendi kutendewa na mtu yeyote.

Akimuwakilisha Waziri Sitta kuzindua Albamu hiyo,iliyokwenda sambamba na harambee iliyowezesha kupatikana kwa shilingi milioni 14.4 zikiwemo ahadi na fedha taslimu, mkuu wa wilaya Ya Kilombero Hassan Masala, alisema Serikali inapenda kuona wananchi wake wanaamini katika imani zao, kwani kwa kufanya hivyo hata serikali itaweza kuwapelekea maendeleo, na kwamba wananchi wamekuwa na kero nyingi sana ambazo haziwezi kutatuliwa kama watu hawatakuwa katika amani.

Nao waimbaji wa injili Eva Mlwati wa KKKT na Rose Mhando wa kanisa la Anglicana, waliahidi kutumia nafasi yao kuendelea kuhubiri amani ili taifa liweze kuwa na amani,ambayo ilihubiriwa pia na baba wa Taifa Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere,na kwamba inasikitisha kuona matendo maovu na yanayotishia uvunjifu wa amani kama milipuko ya mabomu,ufisadi, rushwa na mambo mengine yakiendelea kushika kasi tofauti na nyakati za nyuma.

No comments:

Post a Comment