Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, July 6, 2014

WAFANYABIASHARA WA MAGIMBI, VIAZI, MIHOGO NA NDIZI WAPANDISHA BEI MARADUFU

HAI baadhi ya wakazi wa Bomang’ombe na Kwasadala wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wamelalamikia Wafanyabiashara wa magimbi, viazi, mihogo na ndizi katika masoko hayo kwa kupandisha bei ya vyakula hivyo na pia kupunguza ukubwa wa mafungu ya vyakula hivyo wakati wa mwezi mtukufu wa ramadhani.

Mwaandishi wa mtandao huu aliopata fursa ya kutembelea  masoko hayo ya Bomang’ombe na Kwasadala na kubaini bei ya vyakula imepanda maradufu mara baada ya kuanza mfungo wa Ramadhani.

Wakazi wa maeneo hayo wamelalamikia wafanyabiashara hao kuwa hawawatendei vyema kwa kuwa wanataka kujipatia faida maradufu bila ya kujali kuwa kwa kufanya hivyo wanawaumiza baadhi ya wananchi kwa vile uwezo wao wa kununua bidhaa hizo ni mdogo.

Wanadai kutokana na wafanyabiashara hao kuwa na tamaa hiyo ya kupita kiasi kwa kupandisha bei za vyakula maradufu wamesababisha waliofunga wasifunge kwa amani.

Mmoja wa wakazi wa Bomang’ombe Kibaoni ambaye hakutaka jina lake liandikwe   alisema kuwa wanalazimika kutumia fedha nyingi kununua mafungu mengi ya vyakula hivyo kwa ajili ya futari baada ya mafungu ya viazi, mihogo, magimbi kupunguzwa na wafanyabiashara hao ili kupata faida zaidi.

Na mmoja wa wafanyabiashara hao alisema kuwa wamelazimika  kupandisha bei ya vyakula hivyo kutokana na kuuziwa bei kubwa na wakulima.

Kwa upande wake Anita Nkya ambaye ni mwenyekiti wa soko la Bomang’mbe alikiri kupanda kwa bidhaa hizo na kusema kuwa mahitaji yamekuwa mengi watumiaji wamekuwa wengi hasa katika kipindi hichi cha mfungo wa ramadhani. 
 
Aliendelea kusema awali fungu la viazi, mihogo  lilikuwa likiuzwa kwa shilingi mia tano hadi elfu moja, lakini kwa sasa fungu linauzwa shilingi elfu moja mia tano hadi elfu mbili na kwa mkungu wa ndizi ulikuwa unauzwa shilingi elfu nane hadi elfu kumi, ila kwa sasa unauzwa shilingi elfu kumi na tatu hadi elfu kumi na tano, hivyo kuwaomba wakulima kupunguza bei ya vyakula ili wananchi wapate futari kwa urahisi.

No comments:

Post a Comment