HANDENI wananchi wilayani Handeni mkoani Tanga wameshauriwa
kulitumia dawati la jinsia lililopo katika idara ya polisi kuelezea matatizo
yanayowakabili bila woga ili kuweza kupunguza masuala ya unyanyasaji yanayoendelea
kujitokeza kila siku katika jamii.
Kamanda wa polisi wilaya ya Handeni Zuberi Chembera
alisema hayo ofisini kwake juzi alipokuwa akiongea na mtandao huu na kusema
kuwa wananchi wasiogope kwenda polisi kwani kuna dawati hilo la jinsia na kazi
yake ni kuwasikiliza na kuwasaidia matatizo yanayowakabili.
Alisema dawati hilo kwa kushirikiana na idara nzima
ya polisi, kamati ya ulinzi na usalama na idara za elimu zimejitahidi kutoa
elimu kwa wazazi, wanafunzi na walezi kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wao
ambapo takwimu zinaonesha kuwa wameitikia wito na kwasasa kiwango cha wanafunzi
wanaopata mimba wilayani Handeni kimepungua.
Kamanda Chembera alisema mwaka jana 2013 mwezi Januari hadi mwezi Mei
takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi 22 walipata ujauzito hali iliyosababisha
wanafunzi hao kushindwa kuendelea na masomo, kitu ambacho kimekuwa kikididimiza taaluma yao ila kwa takwimu za
mwaka huu 2014 mwezi Januari mpaka mwezi Mei zinaonesha ni wanafunzi sita tu ndio wameripotiwa katika dawati hilo kuwa na
ujauzito na kesi zao zimeshaanza kufanyiwa kazi.
Alisema mwaka jana 2013 mwezi Januari hadi mwezi Mei kulikuwa na kesi
38 zinazohusu masula ya mimba kwa wanafunzi ambayo ni idadi kubwa sana kwao
lakini mwaka huu zimepungua hadi kufikia 27 hali ambayo inadhihirisha kuwa elimu
inayotolewa kwa wahusika imeeleweka na watoto wanaweza kufanya vizuri.
“Mwaka jana 2013 hadi mwezi Julai tayari
zilisharipotiwa kesi za mimba 22 na kufunguliwa mahakamani kesi 38 lakini
tunaona kuwa kuna mafanikio kwa elimu tunazotoa kwa wahusika kuhusu umuhimu wa
elimu kwa watoto wetu kwani takwimu hizo zimepungua na hadi sasa kesi za mimba
zilizopo ni 6 tu kutoka 22 na zilizopo mahakamani ni 27 kutoka 38 za mwaka jana
haya ni mafanikio kwetu,
Tunawaomba wananchi walitumie dawati la jinsia bila
woga na siri zao zitatunzwa kwa kutoa taarifa za kutoroshwa
wanafunzi, kuozeshwa na masula ya unyanyasaji endapo yatatokea katika maeneo
yao na sisi kama polisi tutawajibika katika eneo letu na kuhakikisha masuala
haya yanakwisha kabisa” alisema Chembera.
Aliongeza kuwa kitu kingine kilichosababisha
kufanikiwa suala hilo la mimba mashuleni ni kampeni ya “NIACHE NISOME”
iliyoanzishwa na mkuu wa wilaya ya Handeni Muhingo Rweyemamu ambayo imekuwa
ikiwasisitiza wanafunzi kuzingatia masomo yao na kusoma kwa bidii.
No comments:
Post a Comment