“KIRUA VUNJO NORTH AMCOS” Yatarajia Kukusanya Shilingi Milioni 4.8 Kwa Mwaka 2014/2015
MOSHI chama cha ushirika wa masoko na
mazao ya kilimo cha Kirua Vunjo Kaskazini, (Kirua Vunjo North Amcos) cha Moshi
Vjijini, mkoani Kilimanjaro, kinatarajia kupata mapato ya ziada ya shilingi
milioni 4.8 katika msimu wa 2014/2015.
Hayo yameelezwa na
mwenyekiti wa chama hicho Bw. John Chaki, wakati akizungumza na wanahabari
mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, hivi karibuni.
“Ziada hii itatokana na
mapato ya jumla ya zaidi ya shilingi milioni 15 tunayotarajia kuyapata katika
kipindi hiki”, alisema na kuongeza kuwa wanachama wa chama hicho tayari
wameridhia kujiunga na mfumo mpya wa kukusanya kahawa kwa kujitegemea.
Aliongeza, “Ili kufanikisha
zoezi la kujitegemea katika mfumo huu mpya, wanachama wamepitisha ukomo wa
madeni wa shilingi milioni 120 kutoka benki ya ushirika mkoani Kilimanjaro,
(KCBL) kwa ajili ya kukusanyia kahawa katika msimu huu mpya”.
Awali meneja masoko wa KCBL
Bw. Asanterabi Msigomba, alisema benki hiyo tayari imeshaandaa mikakati
inayolenga kuviwezesha vyama vya ushirika wa masoko na mazao ya kilimo
vilivyojiunga na mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani.
Aidha alitoa wito kwa vyama
vya ushirika masoko na mazao ya kilimo kujenga tabia ya kuwalipa wakulima fedha
zao punde wanapowasilisha mazao yao ili waweze kujiendeleza ikiwamo kulipa fedha
walizokopa kwa ajili ya kuimarisha kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
“Kosa kubwa ambalo linaweza
kudhoofisha juhudi za kilimo ni kutokumlipa mkulima kwa wakati na wakulima
kuuza mazao nje ya mfumo wa chama, mambo haya hudhoofisha mfumo mzima unaolenga
kuongeza tija katika kilimo”, alionya.
Bw. Msigomba pia alielezea
umuhimu wa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ulioasisiwa na benki hiyo ya
kwanza ya ushirika hapa nchini ambapo alisema tayari taasisi hiyo ishatoa
mafunzo kwa vyama vya ushirika wa masoko na mazao ya kilimo, (Amcos), kuhusu
mfumo huo.
No comments:
Post a Comment