Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, June 19, 2015

BAADA YA ALI KIBA KUCHUKUA TUNZO TANO SASA APEWA UBALOZI WA WANYAMAPORI


Ali Kiba


WIZARA ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na asasi za kimataifa WildAid na African Wildlife Foundation na Balozi mpya wa WildAid muimbaji maarufu Ali Kiba, wamezindua kampeni mpya ya kuongeza ufahamu na kuielimisha jamii kuhusu tatizo sugu la ujangili linaloikabili Tanzania.
Kampeni hii inatarajiwa kuongeza mwamko wa taasisi za kiraia katika kulinda tembo na wanyama wengine.
Tanzania imepoteza asilimia 60 ya tembo wake katika miaka sita iliyopita zaidi kutokana na ujangili kwa ajili ya pembe za ndovu. Wanaonufaika zaidi na pembe za ndovu ni baadhi ya wafanyabiashara haramu wa nchini China na katika nchi nyingine zenye watumiaji wa bidhaa zitokanazo na pembe za ndovu huku Tanzania ikibaki kuwa muathirika wa tatizo hili.
Watalii wengi wanaokuja nchini hupendelea zaidi kuwaona Tembo, na utalii unachangia asilimia 12 ya pato letu la taifa (GDP)”, alisema Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii. “Tembo wetu ni utajiri mkubwa kwa nchi yetu katika njia mbalimbali na serikali yetu imedhamiria kukomesha uhalifu huu. Hata hivyo hatuwezi kufanya jambo hili peke yetu, tunahitaji kupata msaada wa wananchi wote katika jitihada zetu katika kukomesha wizi huu wa urithi wa taifa letu”.
Muimbaji maarufu wa Afrika Mashariki Alikiba ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa kampeni hii alisema. “Ninafurahi kupewa heshima hii na nitatumia nafasi hii kutoa kila mchango ninaoweza kutoa katika jitihada hizi za kulinda wanyama pori wetu”, alisema Ali Kiba. “Tembo wetu wazuri lazima waachwe waweze kuishi katika mazingira yao ya asili badala ya kuishia kuwa pambo kwenye meza ya mtu”, aliongeza Ali Kiba.
Katika utafiti wa hivi karibuni uliohusisha zaidi ya Watanzania 2,000 waishio vijijini na mijini, zaidi ya asilimia 79 walioshiriki walisema kuwa watasikitika endapo tembo watatoweka Tanzania na zaidi ya asilimia 73 walisema wanaamini kuwa tembo ni utambulisho na urithi wa taifa.
“Watanzania wote bila kujali wanapoishi, ni wadau wa rasilimali hii ya wanyama pori”, alisema Peter Knights, Mkurugenzi Mtendaji wa WildAid. Kauli mbiu ya kampeni hii "Ujangili Unatuumiza Sote’ inatukumbusha kuwa wale wote wanaojihusisha na ujangili wa kuua tembo na kusafirisha pembe za tembo hao kimagendo kwenda Asia ya Mashariki wanatuumiza Watanzania sote”.
Dk. Patrick Bergin, Afisa Mtendaji Mkuu wa African Wildlife Foundation, alisisitiza kwamba ujangili unachafua jina la Tanzania nchi ambayo ina sifa ya kuwa na hifadhi kubwa ya tembo.
“Tanzania imekuwa ikijulikana kwa kuwa na makundi makubwa ya tembo ambapo ukijumlisha na Botswana na Zimbabwe utaona kuwa nchi hizi kwa pamoja zina nusu ya tembo wote waliopo barani Afrika,” alisema Bergin. “Hata hivyo, kiwango cha sasa cha ujangili kinatishia kufuta sifa hii ya kipekee. Wakati Watanzania wanazidi kujifunza zaidi kuhusu janga hili kupitia hii kampeni, tunaamini kuwa watashirikiana na sisi kuilinda mali hii adimu.” 
Kampeni hii itatumia redio na televisheni, mitandao ya kijamii, magazeti, mabango na filamu zitakazoonyeshwa maeneo ya wazi ili kuwafikia wananchi wengi iwezekanavyo wakiwemo wakazi wa vijiji vilivyoko ndani ndani.
Video mpya inayomhusisha Ali Kiba na Jacqueline Mengi tayari imetengenezwa na imeonyeshwa kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa kampeni hiyo.


Chanzo: Lensi ya Michezo

No comments:

Post a Comment