CHAMA cha Wanunuzi wa Kahawa Tanzania (TCBA),
kimewajia juu Wabunge wanaomshinikiza Waziri mkuu, Mizengo Pinda atangaze
kupiga marufuku ununuzi wa kahawa mbivu nchini.
Katibu mkuu wa TCBA,Eric Ng’maryo aliwaambia
wanahabari mjini Moshi jana, Waziri mkuu anapaswa kushauriwa vizuri na
wasaidizi wake kwa vile kutoa tamko kama hilo ni kinyume cha sheria.
“nimefuatilia kwa karibu hoja zilizoibuliwa Bungeni
na waheshimiwa Wabunge wawili wa mkoa wa Mbeya lakini namsihi Waziri mkuu kuwa
suala hilo liangaliwe kisheria na si kisiasa”alisema Ng’maryo.
Kwa mujibu wa Ng’maro, biashara ya kahawa nchini
inatawaliwa na sheria ya tasnia ya kahawa ya mwaka 2001 na kanuni zake na kama
ni kuzitengua, ni lazima utaratibu uliozitunga ufuatwe.
Alisema kuwa uamuzi huo wa wadau wote ambao ni
pamoja na wanunuzi binafsi, wakulima wadogo na wakubwa, wasafirishaji nje ya
nchi ndio unaompa nguvu ya kisheria Waziri kutunga kanuni.
Katibu mkuu huyo alisema maamuzi ya wadau ya kutaka
kuendelea kwa biashara ya kahawa mbivu, yalitungiwa kanuni na Waziri wa Kilimo
na kanuni hizo zilipata nguvu ya kisheria Mei 25 mwaka huu.
Ng’maryo alisema kanuni hizo zilitangazwa kwenye
gazeti la serikali kwa G.N namba 187 la Mei 25 na kuhoji”Waziri anahusikaje na
kanuni hizi…haya ni makubaliano ya wadau tusipotoshe umma”.
Kuhusu suala la ununuzi wa kahawa mbivu kuwa
linamnyonya mkulima, Ng’maryo alisema hiyo ni dhana potofu na propaganda chafu
ili kuua ushindani wa kibiashara mkoani Mbeya.
Ng’maryo aliwataka wanaopotosha suala hilo kutokana
na maslahi binafsi waache kuwayumbisha wakulima na wakulima waachwe wenyewe
kuamua wauze kahawa yao katika hatua gani.
Wakati wakichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya
waziri mkuu unaoendelea Bungeni, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na
Rungwe Magharibi, David Mwakyusa walipinga biashara hiyo.
Zambi alienda mbali na kusema hataunga mkono bajeti
hiyo kama hatapata majibu stahiki huku Mwakyusa akitaka Waziri mkuu kupiga
marufuku biashara hiyo wakati akihitimisha hotuba yake.
Wakati hayo yakijiri, taarifa zilizopatikana baadae
jana zilisema wakulima wilayani Mbozi wametuma ujumbe wa watu 15 kwenda kumuona
waziri mkuu wakipinga mapendekezo ya Zambi na Mwakyusa.
No comments:
Post a Comment