Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, July 13, 2012

MBUNGE WA CCM ATIMULIWA BUNGENI...!


 
Florence Majani na
Neville Meena, Dodoma
NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai amemwadhibu Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndungulile kutohudhuria vikao vitatu mfululizo baada ya kushindwa kuthibitisha tuhuma kwamba madiwani wa Halmashauri ya Manispaa Temeke walihongwa ili kuukubali Mradi wa Mji Mpya wa Kigamboni.

Ndugai alitumia kifungu cha 73 (3) ambacho kinampa mamlaka ya kumwadhibu mbunge aliyeshindwa kuthibitisha tuhuma alizozitoa, huku pia akiwa amekaidi kufuta kauli yake kuhusiana na tuhuma hizo.

“Kwa kutumia kifungu namba 73 cha Kanuni za Bunge, hutahudhuria vikao vya Bunge mara tatu mfululizo, askari mtoeni nje,” aliagiza Ndugai.

Awali, Dk Ndungulile alishtakiwa na madiwani wanne wa Kigamboni kwamba aliwatuhumu kupewa rushwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ili waunge mkono mradi wa kuendeleza mji huo mpya wa Kigamboni.

Madiwani hao jana waliliandikia Bunge kukanusha tuhuma zilizotolewa na Dk Ndungulile kuwa walihongwa fedha na

Profesa Tibaijuka ili kufika bungeni

Katika malalamiko yao, madiwani hao ambao walihudhuria kikao cha Bunge hapo juzi wakati Bajeti ya Makadirio ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikisomwa, walipinga madai ya Ndungulile kuwa wakazi wa Kigamboni wamemtuma na kuwa wanaupinga Mradi wa Mji Mpya wa Kigamboni.

Akisoma barua ya malalamiko ya madiwani hao  iliyowasilishwa bungeni, Ndugai alinukuu maandishi katika barua hiyo yaliyosema:

“Sisi madiwani tunakanusha taarifa zilizotolewa na mbunge wetu, Faustine Ndungulile kuwa tulipewa fedha ili kuja bungeni,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Madiwani hao waliendelea kulalamika kwamba, matamshi yaliyotolewa na mbunge huyo yamewadhalilisha na kuondoa imani ya wananchi juu yao kama viongozi, na kuwa wanamtaka aifute kauli yake na kuwaomba radhi.

Sehemu ya barua hiyo pia ilisema hakuna diwani yeyote aliyefika bungeni hapo kwa kupewa fedha na mtu yeyote, bali kwa ridhaa yao wenyewe.

Baada ya kusoma barua hiyo, Ndugai alisema atamtaka mbunge huyo ama kuifuta kauli juu ya madiwani hao au kuthibitisha tuhuma hizo.

“Ndiyo maana, kila siku tunawaonya hapa tusitamke maneno tusiyokuwa na uhakika nayo, wakati mwingine yanaweza kutuweka matatani,” alisema Ndugai.

Juzi, Ndungulile aliipinga vikali Bajeti ya Wizara ya Ardhi  na kumtuhumu ProfesaTibaijuka kuwahonga madiwani hao ili waupigie debe mradi huo ilhali wakazi wa Kigamboni hawautaki.

Alipotakiwa kuthibitisha tuhuma hizo, Ndungulile alisema hakuwataja madiwani hao kwa majina bali alisema madiwani 43 ndiyo waliokuja kwa kuhongwa kwa kutumia fedha za wizara.

“Hata kanuni za Takukuru zinaonyesha kuwa walichokifanya kina mazingira ya waziwazi ya rushwa,” alisema Ndungulile.

 Alifafanua kwamba, mazingira hayo ya rushwa yanakuja baada ya waziri kuwaita madiwani wa Temeke badala ya madiwani wa jimbo lake la Muleba.

Mnyika naye matatani

Kwa upande wake Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika anakabiliwa na madai ya kumtuhumu Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba kwamba ni mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa Fedha za Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Tuhuma dhidi ya Nchemba zilizotolewa na Mnyika, sasa zitapelekwa katika Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Hassan Ngwilizi.

Ndugai alitoa mwongozo huo baada ya Nchemba kuomba mwongozo bungeni, kwa kutumia Kanuni ya 68 (7) na kusema anahitaji Mnyika athibitishe tuhuma hizo kwa kuwa siku saba za kufanya hivyo tayari zimeshapita.

Nchemba alidai kwamba tuhuma hizo hazikuwa za kweli kwani wakati wizi huo unafanyika yeye hakuwa mwajiriwa wa BoT kama Mnyika alivyodai, na kwamba zililenga kumdhalilisha na kumharibia jina kwa wapiga kura wake.

Ndugai alisema Mnyika alifikisha uthibitisho wa maandishi ambao hata hivyo, si uthibitisho kamili bali ni utangulizi tu wa maneno ambayo ndani yake hayathibitishi tuhuma dhidi ya mbunge mwenzake.

“Ni kweli kuwa siku saba alizopewa Mnyika kuthibitisha tuhuma dhidi ya mheshimiwa Nchemba zimepita, lakini tulichopokea si uthibitisho kamili bali ni kama maelezo tu. Kwa hiyo tutalifikisha suala hilo mbele ya Kamati ya Maadili," alisema Ndugai.

Ndugai aliongeza kuwa, wabunge wanaotoa tuhuma bila kuleta uthibitisho waache tabia hizo kwani zinachochea chuki na zinawaondolea wananchi imani kwa viongozi wao.


“Wabunge ni viongozi wakubwa na wanaoaminiwa na wananchi. Tunapodiriki kusema uongo tunajiharibia sifa zetu za uongozi, kama huna uhakika na tuhuma unazozitoa basi usizilete mbele ya Bunge,” alisema.

Hata hivyo, jana mchana Mnyika alisema uamuzi wa Ndugai wa kupeleka suala lake katika Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ulikuwa umepangwa na unakiuka kanuni za Bunge.

Mnyika akizungumza na waandishji wa habari nje ya bunge, alisema ni wazi kwamba Ndugai alikiuka Kanuni za Bunge na kuwa yeye na Nchemba walikuwa wamejipanga kufanya propaganda bungeni.

Alisema, Kanuni ya Bunge ya 73 (3),  inamhusu mbunge ambaye ameshindwa kutoa uthibitisho bungeni katika muda uliopangwa.

Alisema badala yake, Naibu Spika aliamua kulipeleka jambo hilo katika kamati ambayo siyo kazi yake ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge.

Mnyika alisema kamati hiyo kazi yake ni kushughulikia masuala ya wabunge wanaowatuhumu bungeni watu walio nje ya Bunge na kushughulikia migogoro ya kimasilahi.


Akizungumzia uthibitisho wake, Mnyika alisema Jenister Mhagama  aliyekuwa anaongoza kikao siku hiyo, alikurupuka kwa kumtaka alete ushahidi kwa kitu ambacho hakukisema.

“Mimi sikuzitaja tuhuma anazotuhumiwa Mwigulu, nilisema anatuhumiwa na hata pale nilipomtaka Mhagama aniruhusu nizitaje tuhuma zenyewe, hakuniruhusu badala yake akakimbilia kutoa uamuzi kuwa nilete uthibitisho kuwa Mwigulu anahusikaje na EPA.

“Katika barua yangu ya ushahidi kwa Spika, nilipeleka uthibitisho wangu kwa kile nilichokisema na nimenukuu ‘hansard’ (Taarifa rasmi ya bunge), kwa hiyo sijathibitisha kitu ambacho sikukisema,” alisema Mnyika.

Mnyika pia alisema amekata rufaa katika Kamati ya Kanuni kuwashtaki Spika, Naibu Spika na wenyeviti wa Bunge kwa kulinyima Bunge fursa ya kuisimamia Serikali katika mambo muhimu, kwa kisingizo kuwa mambo hayo yapo mahakamani.

Giza lakatisha Bunge

Katika hatua nyingine, Ndugai alijikuta akiahirisha shughuli za Bunge  jana kabla ya wakati, baada ya umeme kukatika na jenereta iliyopo kushindwa kukidhi haja katika jengo hilo.

Umeme ulikatika wakati kikao cha Bunge kikiingia katika shughuli muhimu ya kupitisha makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.


Ndugai alitoa maagizo kuwa Bunge liendelee na shughuli zake katika hali hiyo ya giza, ambapo waziri wa wizara hiyo, Profesa Tibaijuka aliendelea kujibu maswali ya wabunge huku ukumbi ukiwa katika giza totoro.

Kikao kiliendelea gizani kwa takriban  dakika kumi ambapo wabunge watatu walitaka majibu katika hali hiyo ya giza na Profesa Tibaijuka akayajibu katika hali hiyohiyo.

Hata hivyo, hakukuwa na utulivu hasa wakati wabunge wengine walipokuwa wakiuliza maswali yao na wengine kusoma kitabu cha makadirio ya wizara ya bajeti hiyo kwa kutumia simu za mikononi.

Ndipo Ndugai alipoamua kuahirisha kikao hicho hadi leo saa 3:00 asubuhi ambapo Bunge litaendelea kupitisha bajeti hiyo kifungu kwa kifungu.

“Hatutaweza kuendelea katika hali hii, kwa hiyo naahirisha kikao hiki hadi hapo kesho,” alisema.

No comments:

Post a Comment