KILIMANJARO serikali imeanza kusambaza mbegu bora za kisasa za mtama kwa wakulima wilayani
Moshi, mkoani Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kukabiliana na
janga la njaa katika kipindi cha ukame ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kiuchumi.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa wilaya ya Moshi Dkt. Ibrahim
Msengi, wakati akizungumza na waandishi
wa habari ofisini kwake jana Mjini Moshi mkoani hapa ambapo alisema katika
kukabiliana na janga la njaa kwa wananchi serikali imeanza kutoa mbegu hizo bure kwa wakulima.
Dkt. Msengi alisema wilaya
hiyo katika maeneo yake ya tambarare kila mwaka yamekuwa yakikabiliwa na janga
la njaa na kulazimika kupata chakula cha msaada kutoka serikalini kwa aajili ya kunusuru
hali hiyo na kwamba kutokana na suala hilo wilaya hiyo imeanza mchakato wa
kusambaza mbegu bora za zao la mtama
ambalo huvumilia ukame.
Aidha alisema kumekuwa na mashamba darasa ya kilimo cha zao
hilo kwaajili ya kuhamasisha wananchi na wakulima kujihusisha na kilimo cha zao
hilo ambapo kwasasa watu wengi wamehamasika na
wamejitokeza na kutaka kuanza kulima mtama.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kujitokeza na
kujihusiha na kilimo cha zao la mtama kwaajili ya chakula na biashara ili
kuweza kujikwamua katika wimbi la umasikini.
Katika hatua nyingine Dkt. Msengi aliwataka wananchi
kuhifadhi na kutunza chakula walicho nacho katika msimu huu wa mavuno kwaajili
ya kukabiliana na janga la njaa.
No comments:
Post a Comment