KILIMANJARO Naibu Waziri wa Maliasili na Utaliii, Mahmoud Mgimwa,
amewataka waongoza watalii (Tour Guides) kuhakikisha kuwa wana mikataba halali
ya kazi na wamiliki wa makampuni wanayofanyia kazi ili kuepuka kunyonywa haki
zao.
Mgimwa ametoa rai hiyo wakati akitoa nasaha zake katika
mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha waongoza watalii mlima Kilimanjaro (KGA)
kilichofanyika mjini Moshi ambapo Mwenyekiti wa chama hicho, Respicius Baitwa
alimwelezea waziri huyo kuwa, pamoja na ugumu wa kazi yao, baadhi ya wamiliki wa
makapuni ya utalii wamekuwa wakiwanyonya haki zao.
Waziri huyo amewa ahidi waongoza watalii hao wa mlima
Kilimanjaro kuwa, atakutana na chama cha wamiliki wa makapuni ya utalii nchini
(TATO) pamoja na chama cha wamiliki wa
makampuni ya utalii Kilimanjaro (KIATO) ili kuona namna ya kulinda maslahi ya
waongoza watalii hao.
Mgimwa amefafanua kuwa, hifadhi ya mlima Kilimanjaro ndio hifadhi
ambayo inaaingizia serikali mapato makubwa ikilinganishwa na hifadhi nyingine
hivyo kuwataka waongoza watalii hao kufanya kazi zao kwa umakini, uadilifu na
nidhamu ya hali ya juu kwani kwa kutofanya hivyo watalikosesha taifa mapato
makubwa yatokanayo na utalii.
Pia, waziri huyo amewataka wanachama wa KGA kuendeleza umoja
wao ili waweze kusaidiana katika kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo
ukosefu wa vifaa maalumu vya kupandia mlima Kilimanjaro.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa chama cha
waongoza watalii mkoa wa Kilimanjaro, Respicius Baitwa, ameiomba serikali kuingilia
kati viwango vya malipo vinavyotolewa na makapuni ya
utalii, ili kukidhi hali halisi ya kazi
wanazozifanya za kuwaongoza watalii hao.
Amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa vitendea kazi licha
ya kufanya kazi katika mazingira magumu ya kuwaongoza watalii hao.
Kwa upande wake mkuu wa mhifadhi ya KINAPA, Erasto Lufungulo,
waongoza watalii wamekuwa sehemu kubwa
katika kuyatunza mazingira ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro.
Aidha ameongeza kuwa waongoza watalii wamekuwa wakitoa huduma
bora, usalama wa wageni wenyewe hivyo kuwa sehemu ya watumishi wa hifadhi ya mlima
Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment