KILIMANJARO viongozi wa shirikisho la soka nchini TFF, wametakiwa kuondoka maofisini na kwenda
kusaka vipaji vya michezo katika maeneo ya vijijini ambako kuna vipaji
mbalimbali, ili kuweza kuwapata
wachezaji ambao watashiriki katika timu ya vijana ya taifa.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Vijana CCM, Ester Bulaya
wakati alipokuwa akifunga mashindano ya John Samwel Malecela Cup 2014, ambayo
yalishirikisha timu 16 za kata na timu 19 kutoka shule za sekondari zilizopo
katika jimbo la Same Mashariki , ambapo mashindano hayo yaliandaliwa na Mbunge
wa jimbo hilo, Anne Kilango Malecela.
Mhe, Bulaya amesema mashindano hayo yametoa fursa kwa
vijana kuibua vipaji vyao, na hivyo kutoa rai kwa Rais wa TFF, kuacha kuendelea
kukaa ofisini na badala yake aende vijijini ambako kuna vipaji vingi vya
wachezaji ambao ni vijana.
Bulaya amesema viongozi wa TFF, wasikae ofisini, waende
kutafuta vijana ambapo wataweza kushiriki kwenye timu za taifa za vijana, akili
zao zisiishie kwenye timu za Simba na Yanga pekee.
Amesema TFF endepo kama wangekuwa wanatoka na kwenda
kusaka vipaji vilivyopo katika maeneo ya vijiji wangeweza kupata wachezaji
wazuri ambao wangeweza kuichezea timu ya taifa ya vijana na kuweza kuitangaza
nchini katika medani za michezo.
Mashindano hayo ambayo yalidhaminiwa na Mbunge wa
jimbo hilo Anne Kilango Malecela, kwa lengo la kuibua vipaji kwa vijana sanjari na
kuwaelimisha vijana kujiepusha na vitendo viovu katika jamii yameleta furaha kubwa kwa mashabiki wa timu
hizo.
Kilango amesema "nia ni kuweza kuwaunganisha vijana wa
jimbo langu ili kuibua vipaji walivyo navyo ili kupata wachezaji bora katika
michezo mbalimbali."
Aidha katika michezo hiyo Mbunge huyo ametoa zawadi
mbalimbali kwa timu zote zilizoshiriki michezo hiyo huku mshindi wa kwanza
akiondoka na kitita cha shilingi laki saba na kombe.
Timu ya soka ya Maore ilifanikiwa kuchukua kombe hilo baada ya
kuichapa timu ya Kihurio kwa goli 1-0 kwa
timu za Kata katika dimba la fainali lilochezwa katika viwanja vya Mamba Myamba wilayani Same.
Katika upande wa timu za sekondari, timu ya Parane
iliibuka mshindi katika fainali hiyo baada ya kuifunga timu ya Ntenga sekondari Magori 2-0 na kuifanya timu
ya Parane kushika nafasi ya pili na
kuzawadiwa kikombe na pesa taslimu kiasi cha shilingi laki tano (500,000),huku timu ya Ntenga
ikijinyakulia kikombe na pesa taslimu kiasi cha shilingi laki tatu (300,000).
No comments:
Post a Comment